WAPIGA DEBE WAPIGWA KUPIGWA DAR

BAADA ya kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa abiria kuhusu wapiga debe katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo, jijini Dar es Salaam Kampuni ya Start My Safari, imeahidi kutatua changamoto hizo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Kampuni hiyo imedai kuwa kwa kipindi kirefu imekuwa ikiziona kero wanazopata abiria wanaokwenda mikoani kutoka kwa baadhi ya wapiga debe wa mabasi wasio waaminifu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampuni hiyo, Meneja Uendelezaji Biashara wa kampuni hiyo, George Mlambaka, alisema imekuwa ikitoa huduma ya kukata tiketi za mabasi kwa njia ya kielektroniki.
“Tunafanya kazi na kampuni za mabasi zaidi ya 25. Pia leo tunazindua kifaa ambacho mawakala wetu watakuwa wanakitumia kuuza tiketi, lakini pia watu wa mabasi watakuwa wanakitumia,” amesema Mlambala.
Amesema katika dunia ya leo watu wote wanahamia kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki, hivyo kupitia simu za mkononi Watanzania wanaotaka kukata tiketi za mabasi wana uwezo wa kufanya hivyo wakiwa mahali popote.
Mtendaji wa Huduma kwa Wateja, Dorice Kini, alisema kampuni hiyo kwa sasa imefanikiwa kuwa na mabasi yanayoenda nje ya nchi katika programu yao ya simu itakayomsaidia mteja kukata tiketi akiwa popote.
"Ukipata safari ya ghafla utafungua mfumo wa kielektroniki kwenye simu ambao utakuletea orodha ya mabasi yaliyopo na nauli za halali kama zilivyopangwa na mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),” amesema Mlambala.
Alisema huduma hiyo si kwa watumiaji wa simu pekee, bali hata wasio na simu.
Alifafanua kuwa kupitia huduma hiyo wamedhamiria kuwaondolea Watanzania usumbufu wa kulanguliwa tiketi kwa bei za juu. Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Start My Safari, Joshua Sewe, alisema baada ya mteja kukata tiketi, kitengo hicho kinaendelea kumfuatilia kujua iwapo amefika salama aendako.

Hakuna maoni